Mwisho wa zama kwa Angela Merkel

Chama tawala nchini Ujerumani, CDU, chapata kiongozi mpya

Mwisho wa zama kwa Angela Merkel

 

Chama tawala nchini Ujerumani CDU kimefanya mabadiliko ya uongozi wa juu na kiongozi wa chama hicho sasa ni  Annegret Kramp-Karrenbauer. Nafasi hiyo ya uongozi wa chama cha CDU ilikuwa ikishikiliwa na kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye katika uchaguzi mkuu wa 31 wa chama hicho  hakuwania tena.

Bi Karrenbauer alikuwa akishikilia nafasi ya katibu mkuu wa chama hicho kabla ya uchaguzi huo. Katika uchaguzi mkuu huo uliofanyika mjini Hamburg, Bi Karrenbauer aliwashinda mbunge wa zamani Friedrich Merz pamoja na waziri wa afya Jens Spahn ambao pia walikuwa wakiwania nafasi hiyo.

Katika awamu ya kwanza ya uchaguzi huo kati ya kura 999 zilizopigwa bi Kramp-Karrenbauer, alipata kura 450 wakti Merz alipata kura 392 na Spahn alipata kura 157. Uchaguzi huo ilibidi uende mzunguko wa pili kutokana na kwamba hakuna mgombea aliyefikisha nusu ya kura zote zilizopigwa.

Katika mzunguko wa pili wagombea wa kwanza waliokuwa na kura nyingi kwenye mzunguko wa kwanza walishindana na matokeo yake ni kati ya kura 999 zilizopigwa Kramp-Karrenbauer, alipata kura 517 na kuchaguliwa kuwa kiongozi mpya wa chama hicho tawala nchini Ujerumani cha CDU. Merz kwenye mzunguk wa pili alipata kura 482.

Annegret Kramp-Karrenbauer anakuwa kiongozi mkuu wa nane wa chama hicho baada ya Angela Merkel.

Baadaya uchaguzi huo Kramp-Karrenbauer, alipanda jukwaani kutoa neno la shukrani na pia kupokea salamu za pongezi.

Merkel anaachia madaraka katika chama hicho baada ya kukiongoza kwa miaka 18. Mnamo mwezi Oktoba alitangaza hatogombea tena kuongoza chama hicho ila ataendelea kuwa Kansela wa Ujerumani mpaka mwisho wa muhula.

 

 

 Habari Zinazohusiana